Tanzania emblem
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

JESHI LA KUJENGA TAIFA -JKT

Mheshimiwa Mgumba Aagiza Bodi ya Mkonge kushirikiana na JKT Mgambo.

03 Oct, 2022
Mheshimiwa Mgumba Aagiza Bodi ya Mkonge kushirikiana na JKT Mgambo.

Mkuu wa mkoa wa Tanga Mhe. Omary Mgumba ameelekeza Mkurugenzi wa Bodi ya Mkonge ambaye makao Makuu yake yapo Tanga, kwenda katika Kikosi cha JKT Mgambo kilichopo katika wilaya ya Handeni, mkoani humo ili kuongeza ushauri wa kitaalam kufuatia mpango wa uanzishwaji wa shamba kubwa la mkonge.

Hatua hiyo imejiri wakati alipofanya ziara ya kukagua shamba lenye ukubwa wa ekari 200 la mkonge, pamoja na kitalu kilichooteshwa miche ya mikonge zaidi ya laki moja na arobaini katika kikosi cha JKT Mgambo.

Sambamba na hilo, Mheshimiwa Mgumba amepongeza juhudi za JKT kupitia kikosi hicho kwa kuendeleza zao la mkonge, huku akiahidi kuwa serikali ya mkoa kupitia wataalam wake itaendelea kutoa huduma katika shamba hilo la JKT Mgambo lililopo mkoani Tanga.

Mheshimiwa Mgumba amesisitiza kuwa, kwa sasa JKT ni wakulima wa kati ambao wanaelekea kuwa wakulima wakubwa hapa nchini, hivyo ni lazima wahudumiwe kwa ukaribu kwa kuzingatia taaluma, ujuzi na teknolojia ya zao la mkonge.

Aidha, katika kukuza sekta ya kilimo nchini, Mheshimiwa Mgumba amependekeza kuwepo na Kituo cha Rasilimia Kilimo kwenye kila kambi ili vitumike kama mashamba darasa kwa vijana wanaopatiwa mafunzo ya JKT na jamii inayozunguka maeneo ya makambi ya Jeshi hilo.

Mheshimiwa Mgumba amesema hatua hiyo itawezesha vijana wa JKT na wakulima kwa ujumla kupata huduna zinazohusu masuala ya kilimo cha mazao mbalimbali kwa kipindi chote cha mwaka ikiwemo zao la mkonge.

 JKT kupitia kikosi chake cha Mgambo kilichopo wilayani Handeni mkoa wa Tanga, kimeweka lengo la kulima zao la mkonge ekari 1000 ifikapo mwaka 2025 kwa kulima ekari elfu mbili kila mwaka.

Jeshi la Kujenga Taifa katika utekelezaji wa majumu yake yakiwemo ya malezi ya vijana na uzalishaji mali kupitia makambi ya jeshi hilo, limeendelea kutekeleza maelekezo ya Serikali ya kuhakikisha mazao ya kimkakati ikiwemo mkonge yanapewa kipaumbele katika uzalishaji wake.