Tanzania emblem
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

JESHI LA KUJENGA TAIFA -JKT

JKT Lashiriki Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani 2022

07 Jun, 2022
JKT Lashiriki Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani 2022

JKT Lashiriki Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani 2022

 

Jeshi la kujenga Taifa (JKT) pamoja na Majukumu yake ya Malezi ya Vijana, Uzalishajimali na Ulinzi pia limekuwa ni mdau mkubwa wa uhifadhi na utunzaji wa mazingira  katika maeneo yake ya vikosi na Makambi hapa nchini.

 

Shughuli za uzalishaji zinazofanywa na JKT  zimekuwa zikisaidia uhifadhi na utunzaji wa mazingira  hali inayochochea Vijana wanaopatiwa mafunzo ya JKT kujifunza umuhimu wa uhifadhi na utunzaji wa mazingira kwa manufaa ya Jeshi na Taifa kwa ujumla.

 

Mwaka huu Maadhimisho ya siku ya Mazingira Duniani yamefanyika kwenye viwanja vya Jakaya Kikwete Convection  kuanzia tarehe Mosi Juni, 2022  na kilele chake kilikuwa tarehe 5 Juni, 2022.

 

Akizungumzia ushiriki wa JKT katika Maadhimisho hayo kwa mwaka huu, Mwenyekiti wa Kamati ya  Maadhimisho  JKT Kanali Amosi Mollo amesema Jeshi hilo limeshiriki maadhimisho hayo ili kutoa elimu kwa wananchi kupitia shughuli zake ikiwemo kilimo cha miti na  uzalishaji mali zinavyofanywa katika vikosi vyake, ambazo licha ya kuongeza kipato kupitia mazao yake, lakini pia zinasaidia kuhifadhi na kutunza mazingira.

 

Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati ya Maandalizi ya Maadhimisho hayo kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira (NEMC), Mhandisi Juma Limbo amelipongeza JKT kwa namana linavyoshirikiana na ofisi yake katika kuhifadhi na kutunza mazingira.

 

Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira kupitia Baraza la Taifa la Mazingira imekuwa likiratibu maandalizi ya siku ya mazingira Duniani kila mwaka ifikapo tarehe 5 Juni, huku JKT likiwa na mchango mkubwa wa utunzaji mazingira kwa kufanya shughuli za uzalishaji zinazosaidia uhifadhi na utunzaji wa mazingira.

 

Katika Vikosi na Makambi ya JKT  Maafisa, Askari, Vijana na Watumishi wa Umma mara kwa mara wamekuwa wakihimizwa kupanda miti katika maeneo yao ikiwa ni njia mojawapo ya uhifadhi na utunzaji wa mazingira.