Jumanne, 17 Mei 2022

Historia ya Jeshi la Kujenga Taifa

 

Kuanzishwa kwa JKT, kulitokana na mawazo ya Umoja wa Vijana wa Chama cha TANU (TANU Youth League), katika Mkutano wao Mkuu uliofanyika mjini Tabora tarehe 25 Aug 62, chini ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja huo, hayati Joseph Nyerere.

 

Tarehe 19 Apr 63, Baraza la Mawaziri la Tanganyika chini ya Rais wa Jamhuri ya Tanganyika na Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere, lilipitisha Azimio la umoja wa vijana wa TANU na kuamua kwa kauli moja kuazishwa JKT mnamo tarehe 10 Jul 1963. Kundi la kwanza lilipata mafunzo katika kambi ya Mgulani Dar es salaam likiwa na jumla ya vijana 11 toka wilaya 11 tofauti.

 

Vijana hao wa mwanzo walikuwa makatibu wa umoja wa vijana ambao walikwishapelekwa na TANU huko Yugoslavia mwaka 1962, kuchukua mafunzo ya uongozi wa vijana. Baadhi ya vijana hao watangulizi ni Bi. Z. Kiango, Bw. S. Chale, Bw. P. Lwegarulira, Bw. R. Kamba, Bw. H. Ngalason, Bw, J.Ndimugwango, Bi. M. Mhando (Senior Guide), Bw. D. S. Msilu (Master), Mr ES Mwakyambiki, (Senior Master) na Mr AI Msonge (Master), Mr LM Mitande.

 

Ulipofika mwezi Agosti, 1963 kikundi kingine cha watu watano kikiwa na Bw. S. Desai, Bw. E. Simkone, Bw. J. Mwanimlele (Asst Master) na Bw. A. A Moyo (Asst Master) kilijiunga na kupata pia mafunzo ya uongozi.

 

Kwenye uzinduzi wa JKT, Mwalimu Nyerere alisema Umuhimu wa JKT unatokana na Taifa kuhitaji huduma ya vijana na vijana kuitikia wito huo wa kulitumikia Taifa lao kwa jukumu lolote lihitajiwalo.

SHERIA YA KUANZISHWA KWA JESHI LA KUJENGA TAIFA NA MAREKEBISHO YAKE

Jeshi la Kujenga Taifa lilianzishwa kwa sheria ya Jeshi la Kujenga Taifa (Nationa Service Act) ambayo ni sheria No 16 ya mwaka 1964. Sheria hii inatoa uwezo wa Jeshi la Kujenga Taifa kuandikisha vijana wa kulitumikia Jeshi hilo. Aidha, sheria hii imeendelea kufanyiwa marekebisho kutokana na mahitajio na baadhi ya marekebisho hayo ni:-

1. Marekebisho ya mwaka 1966

  • Tangu lilipoasisiwa JKT lilikuwa linaandikisha vijana wa kujitolea wenye elimu ya darasa la saba tu. Ilipofika mwaka 1966, ilionekana kuwa, kuna umuhimu wa vijana wasomi wenye elimu zaidi ya kidato cha nne kulitumikia JKT. Hivyo, sheria ilirekebishwa ili kulipa JKT nguvu za kisheria ili liweze kuandikisha vijana wenye taaluma zaidi ya kidato cha nne kwa mujibu wa sheria (Compulsory).
  • Marekebisho mengine ni ya mwaka 1975 ambapo, ili kuimarisha ulinzi wa Taifa, JKT liliungana rasmi na JWTZ mwaka 1975 hivyo kulifanya JKT kuwa moja ya Kamandi zilizochini ya JWTZ. Sambamba na marekebisho hayo, shughuli za JKT ziliwekwa bayana kuwa ni:-

a.Kuwafundisha vijana wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kulitumikia Taifa katika nyanja za kijamii, maendeleo ya uchumi na ulinzi wa Taifa.
b. Kutoa mafunzo ya msingi ya Jeshi kwa vijana kwa lengo la kuwawezesha vijana hao kufikia sifa ya kujiunga katika vyombo vya Ulinzi na Usalama JWTZ, Polisi, Usalama wa Taifa na Magereza.
c Kushiriki kikamilifu katika medani ya ulinzi wa Taifa.

  • Japokuwa JKT katika shughuli za malezi ya vijana lilijihusisha na uzalishaji mali pia, shughuli hii ilipata nguvu zaidi mwaka 1981 pale ambapo Shirika la Uzalishaji Mali au kwa kifupi SUMA JKT lilianzishwa kisheria kupitia “The Corporation Sole Establishment Act”.of 1974 Awali, nia ya kuanzishwa SUMA JKT ilikuwa ni kusaidia miradi ambayo ilikuwa na uwezo mkubwa wa uzalishaji ili iweze kuzalisha zaidi na kwa faida na hivyo kuisaidia serikali katika kupunguza matumizi katika kuendesha shughuli za JKT.

Hawa ni vijana wa kwanza kunufaika na mafunzo ya JKT walikuwa jumla yao kumi na moja,wengine wametangulia mbele za haki wamebakia Brigedia (Mstaafu) Dismas Msilu na Bi Zainabu Kiango.

 

 

Uadilifu

JKT huwajenga vijana kuwa waaminifu, wakweli na wakutegemewa na Taifa

Umoja na Mshikamano

Kuandaa vijana kuwa jamii yenye mshikamano na umoja wa kitaifa bila kujali itikadi zao za kitamaduni, kisiasa na kidini.

Kujitolea

Kuandaa vijana kuwa na moyo wa kujituma na kujitolea.

Uzalendo

Huwaandaa vijana wawe na moyo wa uzalendo, udugu na kuipenda nchi yao.

Nidhamu

Kuwafundisha vijana kuwa watiifu na wenye heshima.

Kupenda kazi

Kuwaanda vijana kuwa jamii yenye kutekeleza wajibu na moyo wa kupenda kufanya kazi