TAARIFA KWA UMMA
VIJANA KUCHUKUA TAHADHARI NA KUFUATA SHERIA ZA USALAMA BARABARANI
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Limekuwa likitoa taarifa kwa umma na kuwaita Vijana wa Kitanzania kutoka Mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani kujiunga na Mafunzo ya JKT kwa Kujitolea na Kwa Mujibu wa Sheria kila mwaka wa Fedha.
Kutokana na Makambi ya JKT kutawanyika nchi nzima Vijana hao hulazimika kusafiri kutoka Mkoa mmoja kwenda Mkoa mwingine kwa kutumia usafiri wa Barabara na Reli, Na wanapofika vituo vikuu vya mabasi ama Reli, Vijana hao badala ya kutumia usafiri wa Umma (Daladala) ili kuwafikisha katika Makambi ya JKT waliyopangiwa, Baadhi hutumia usafiri wa Pikipiki maarufu kwa jina la Bodaboda, Usafiri ambao hauna uhakika na mara nyingi umekuwa ukisababisha ajali zinazopelekea Ulemavu wa kudumu ama Vifo.
JKT linapenda kuwashauri wazazi na walezi wa Vijana wanaoitwa kujiunga na Mafunzo ya JKT na kupaswa kusafiri, Kuwafuatilia hatua kwa hatua wawapo safarini na kuhakikisha vijana wao wamefika salama katika makambi ya JKT waliyopangiwa.
Aidha, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) linatoa ushauri kwa Wazazi na Walezi wa Vijana kuwapa Vijana wao elimu ya kutosha ya sheria na taratibu za usalama barabarani wawapo safarini sambamba na kuwakumbusha kuchukua Tahadhari za matumizi ya vyombo vya moto visivyo salama sana kwa maisha yao.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Habari na Uhusiano,
Makao Makuu ya JKT,
Tarehe 24 Jun 2021.